Kwa niaba ya wanachama wa Chama cha Uwindaji wa Wenyeji na Uhifadhi TACHA (Tanzania  Conservation and Local Hunters Association), tunapenda kutoa salaamu zetu za rambrambi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Chama Tawala cha CCM na Serikali yake pamoja na wa Tanzania wote kwa msiba huu mzito wa kuondokewa na Rais wetu mpendwa Dr John Pombe Joseph Magufuli. Tunakiri pasipo shaka kwamba taifa letu na Africa kwa ujumla limempoteza kiongozi.

Aliyeendeleza, kujenga na kusimamia misingi imara ya kiuchumi, kijamii na kisiasa katika kuwaletea maendeleo wananchi wake. Aliyafanya haya kwa ujasiri na kwa uadilifu mkubwa na matokeo yake yamekua yanaonekana kila uchao.

Sisi kama Watanzania tutamkumbuka kwa mengi na hasa maendeleo makubwa katika miundo mbinu ya kiuchumi na utendaji Serikalini. Kama wanachama wa TACHA tunamshukuru na daima tutamkumbuka kwa kutukumbusha Wa Tanzania kwamba rasilimali zote ikiwa ni pamoja na wanyama pori ni za Watanzania wote na wanastahili na kwa kweli ni lazima wanufaike nazo na inapowezekana wazitumie ikiwa ni pamoja na kupata kitoweo.

Wakati tunamtakia kila la kheri Rais wetu mpya mama Samia Suluhu Hassan katika kutuongoza na kuendeleza yale yote mema aliyotuachia Mwanamwema wetu Dr John Pombe Joseph Magufulu, tunammwomba Mwenyezi Mungu amjalie neema, hekima, na busara; pamoja na moyo wa imani, ujasiri, upendo, na ukarimu katika kutuongoza ili amani, umoja na mshikamano wetu uendelee kushamiri na kutuwezesha kupata maendeleo makubwa zaidi ya kijamii na kiuchumi.

Bwana ametoa, Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe